Sunday, March 10, 2013

MUHIDINI MWALIMU GURUMO ‘JEMBE’ LINAUMWA’

MUHIDINI  MWALIMU  GURUMO
            JEMBE’ LINAUMWA’

Nov./20/2012

MUHIDINI MWALIMU GURUMO ni mwanamuziki aliyetumikia nchi hii kwa ufanisi mkubwa toka miaka ya 1960, lakini hadi leo yupo katika dimbwi la ufukara uliokithiri.
Katika kipindi chote hicho Mzee Gurumo ametunga nyimbo nyingi zinazoelimisha jamii kuhusu kufanya kazi kwa juhudi na maarifa, kulinda uhuru wa nchi, kudumisha usawa, haki na amani pamoja na kuwaasa wazazi kutumiza wajibu wao kwa kulea watoto  na vijana  kutimiza wajibu wao.
Licha ya sifa zilizoainishwa hapo juu, mzee Gurumo hakuwahi kukumbukwa kwa lolote pamoja na mchango wake mkubwa kwa taifa hili tangia uhuru wa nchi hii mwaka 1961.
Hatimaye kwa mara ya kwanza Mzee Gurumo amekumbukwa kwa kutunukiwa nishani ya heshima ya Muungano na rais Jakaya Kikwete, siku ya maadhimisho ya miaka 51 ya uhuru wa Tanzania Bara, zilizofanyika kwenye uwanja wa uhuru Desemba 09, 2012 Jijini Dar es Salaam.
Gurumo alivishwa nishani hiyo na rais Jakaya Kikwete ambaye aliwatunuku pia wanamuziki wengine watatu, msanii wa maigizo na mwanariadha mkongwe katika viwanja vya Ikulu, jiji Dar es Salaam.
Wasanii wengine waliotunukiwa siku hiyo ni pamoja na kiongozi wa zamani wa Dar. International, Marijani Rajabu, mwimbaji mkongwe wa taarabu, Fatuma Baraka ‘Bi. Kidude’, msanii wa maigizo ya filamu Fundi Said ‘Mzee Kipara’ na  mwanariadha mkongwe, John Steven Akwari.
Baada ya kuvishwa nishani hiyo, Mzee Gurumo alionyesha furaha yake na kumshukuru rais Kikwete na wananchi kwa ujumla kwa kutambua kazi yake ambayo alisema iwe changamoto kwa vijana kutambua kuwa muziki  si  kwa ajili mapenzi pekee, bali kila kitu kinachoihusu jamii.
Mwandishi wa  habari hii  alifika nyumbani kwa Mzee Gurumo  huko  Makuburi, Ubungo ambapo alielezea historia yake na akasema haijui tarehe kamili aliyozaliwa. Anasema kwamba anafahamu kuwa alizaliwa katika  Kijiji cha Masaki, Wilaya ya Kisarawe mkoa wa Pwani mwaka 1940.
Ni  mwanamuziki mkongwe mwenye historia  ndefu katika tasnia ya muziki Afrika Mashariki   na hata nchi  zilizo chini ya Jangwa la Sahara.
Sifa kubwa aliyonayo Mzee Gurumo ni ile ya toka aanze kupiga muziki miaka 52 iliyopita, hakuwahi kupumzika ila mwezi wa mtukufu wa Ramadhani ama awe anaumwa. Kila siku za kazi hakukosa jukwaani.
Rekodi ya sifa hiyo ingeliweza kuvunjwa na mkongwe Salimu Zahoro, ambaye alimtangulia Gurumo katika muziki, akipiga katika bendi ya Kiko Kids ya mjini Tabora. Lakini baada ya bendi hiyo kufa, Mzee Salimu Zahoro  alipumzika mambo ya muziki kwa takriban miaka 20, hadi alipojiunga na bendi ya  Shikamoo Jazz.
Hivi sasa Mzee huyu  ana umri wa zaidi ya miaka 70,  ameshatoa mchango mkubwa katika nchi hii kupitia tungo za nyimbo zake zisizopungua  1, 000 zilizojaa ujumbe mzito kwa jamii.
Mzee Gurumo anailezea afya yake kwa sasa kuwa si nzuri, akisumbiliwa na maradhi yaliyopelekea yeye  kulazwa katika kitengo cha wagojwa mahututi (ICU) katika hosiptali ya Muhimbili.
Kwa masikitiko makubwa mzee huyo anasema ufukara alionao, amefikia hatua ya kuwatamani wanamuziki wa kizazi kipya na taarabu, kuwa wana mafanikio makubwa kimaisha.
Gurumo akafika mbali zaidi kwa kusema mafanikio yao ni  kwa vile soko la sasa limewapokea vyema na yeye kujisikia wivu kuwaona vijana wakiendesha maisha mazuri wakiwa na magari ya kifahari wakati yeye akitembea kwa miguu.
“Hata kwenda Hospitali Muhimbili kutibiwa, ninatumia  usafiri wa daladala licha ya muda mrefu nilioutumia katika muziki” anasikitika mzee Gurumo.
Mke wa mzee Gurumo  Pili  Kitwana alitoa dukuduku lake akisema kwamba yeye binafsi huwa anaumia roho wanapokuwa kwenye daladala  akimpeleka mumewe  hospitali, abiria  wengine huwashangaa. Lakini anasisitiza kwa kusema wana haki ya kuwashangaa  kufuatia jina kubwa la mume wake ambaye kwa hali ya kawaida hakustahili kutumia usafiri wa daladala.
Mama huyo ambaye aliolewa na Muhidini Maalimu  Gurumo mwaka 1967, walipata watoto wanne akina Mariamu, Mwalimu, Omar na Mwazani. Anamtaja  Binti yao wa kwanza Mariamu kwamba amefuata nyayo za Baba yake za usanii japo anaimba nyimbo za kizazi kipya.
Mkewe Pili, akaenda mbali zaidi akisema kwamba  laiti  kama angelikuwa na uwezo, angemtaka mumewe apumzike na masuala ya muziki baada ya kuutumikia kwa zaidi ya miaka 50 pasipo kupata mafanikio ya maana.
Mzee Gurumo mwimbaji mwenye sauti isiyoigika, anakiri fani yake ya muziki imemsaidia kufahamiana na watu wengi  wakiwemo viongozi  mbalimbali hapa nchini  akiwemo rais Jakaya Kikwete.
Anakiri kitendo cha rais Kikwete kuacha kazi zake akifuatana na mkewe, mama Salma kuja kumjulia hali, pia kumsaidia katika matibabu wakati alipokuwa amelazwa katika Hospitali ya Muhimbili kwamba kulimfariji  sana.
Muhidini Gurumo anasema baada ya ujio wa rais Kikwete hapo Muhimbili, huduma zilizofuatia toka kwa  madaktari na manesi zilikuwa ‘Baabu’ kubwa.
Hivi sasa amepewa Daktari maalumu wa kuiangalia afya yake kila aendapo hospitalini humo.
Gurumo mwenye uso wenye bashasha licha ya kudhoofu kiafya, hakukosa kutoa shukurani za dhati kwa mmiliki wa Kampuni African Stars Entertainment Tanzania (ASET),  Asha Baraka  kwa kuandaa onyesho maalumu kwa ajili ya kumchangia pesa.
“Asha Baraka namshukuru sana aliniletea shilingi milioni mbili ambazo zilinisaidia sana katika matibabu”  anasema Mzee Gurumo.
Gwiji huyu ndiye muasisi wa mitindo ya ‘Msondo’ ‘Sikinde’ na ‘Ndekule’ katika bendi za NUTA Jazz, JUWATA, OTTU, Mlimani Park na Orchestra Safari Sound (OSS).
Mwenyewe anasema mitindo hiyo ilitokana  na ngoma za asili ya kabila lake la Kizaramo ambazo mama yake mzazi  alikuwa gwiji wa kuimba na kucheza enzi zake.
Gurumo alianza muziki akiwa na miaka 12 lakini muziki  wa dansi alianza rasmi mwaka 1961, baada ya  kumaliza elimu ya koroani katika madrasa ambako alikuwa hodari wa kughani na kuimbaji kwa ustadi mkubwa Kaswida.
Bendi yake ya kwanza ilikuwa Kilimanjaro Chacha iliyokuwa ya ikiongozwa na Mkurugenzi  wa bendi anamtaja kwa jina la  Samwel Machango. Aidha  anasema alipofika hapo, alipokelewa na Salumu Monde ambaye alikuwa mpigaji wa gita la rhythm. Anakiri kwamba wote wawili walimpa ujasiri wa jinsi ya kulitawala Jukwaa na vilevile kwa juhudi zake binafsi alijifunza kupiga Saxophone.
Bendi hiyo ilikuwa na makao makuu katika ukumbi wa Amana maeneo ya Ilala, jijini Dar es Salaam.
Mzee Gurumo anakumbuka baadhi ya nyimbo alizoimba katika bendi yake ya kwanza ukiwamo wa ‘Nilipoingia Bar watu walinionea kijicho’ Anasema  hawezi kuisahau siku ambayo kwa mara ya kwanza alianza kupata pesa aliyoitolea jasho lake ilikuwa ni shilingi  tano  baada ya onyesho hilo.
Mwaka 1962 kiongozi wa bendi ya Kilwa Jazz Ahmed Kipande alimrubuni kwa kumpa Shilingi mia mbili ili ajiunge na bendi yake. Anasema Shilingi mia mbili miaka hiyo ilikuwa na thamani kubwa sana naye alipokea na kukubali kujiunga na Kilwa Jazz.
Mzee Gurumo anatabanaisha kwamba uongozi  wa  Ahmed Kipande, Duncan Njilima na Juma Mrisho ‘Ngulimba wa Ngulimba’ hawakumtendea haki iliyostahili na  baada ya  mwaka kupita  akaamua kutafuta bendi nyingine. Alifanikiwa kupata bendi ambayo ilikuwa ndogo kuliko Kilwa jazz  ikiitwa Rufiji jazz mwaka 1963.
Mwaka 1964  Gurumo aliitwa na uongozi wa NUTA Jazz ili akubali kuwa muanzilishi wa bendi hiyo na aliungana na wanamuziki wengine akina Hamis Sama, Mnenge Ramadhani na Wilfred  Boniface.
Nyimbo zake za kwanza kurekodi akiwa na NUTA Jazz zilikuwa Baba Nyerere wimbo uliokuwa ukimsifia Mwalimu Nyerere kwa kuleta Uhuru wa Tanganyika. Nyingine zilikuwa Kilimo ni kazi yetu na Mwengele.
Mzee Gurumo pamoja na uzee alionao bado kumbukumbu kichawani zijemjaa. Anakumbuka mwaka 1966 mwanamuziki mwingine mahiri John Simon alijiunga na bendi yao ya NUTA Jazz na anamtaja mpiga Solo, Ahmed Omar kuwa ndiye aliyechaguliwa kuwa Kiongozi wa NUTA Jazz.
NUTA jazz alikuwa ikimilikiwa   Chama cha Wafanyakzi  ambacho baadaye kikawa JUWATA, OTTU, TFTU hadi TUCTA.
Wakati wakiwa na TUCTA mishahara yao ilikuwa duni kiasi cha kushindwa kijikimu kimaisha, hivyo kwa pamoja wanamuziki hao wakajipanga kwa kununua vyombo vyao vya muziki kidogo kidogo hadi wakatimiza adhma yao ya kujitegemea. Ndipo bendi ya Msondo Ngoma ilopanzisha  ikilibakiza jina la Msondo kwa kuienzi staili iliyowapa  umaarufu.
Mwaka 1978 Gurumo alihamia bendi ya Mlimani Park Orchestra ‘Wana Sikinde ngoma ya ukae’ na akawa kiongozi wa bendi hiyo baada ya muda mfupi alitunga nyimbo zikiwemo Baba na Mama na Weekend.
Akiwa na bendi hiyo maisha yake yalianza kubadilika na kuwa mazuri kufuatia malipo na maslahi ya kuridhisha aliyokuwa akilipwa na uongozi wa Mlimani Park.
Anajigamba kwamba maslahi hayo ndiyo uliofikisha kujenga nyumba yake na kunua eneo la shamba maeneo ya Masaki Wilayani Kisarawe mkoa wa Pwani  na kuwapeleka watoto wake katika Shule nzuri.
Anasema hatoweza kuwasahau wanamuziki alioshirikiana nao kwa karibu akiwemo aliyekuwa kiongozi msaidizi Comas  Tobias Chidumule, Joseph Bartholomew Mlenga ‘King Spoiler’ na Abdallah Gama.
Pamoja na kipato alichokuwa akikipata Mlimani Park Orchestra, mwaka 1985 mfanyabiashara maaraufu jijini Dar- es -Salaam  Hugo Kisima, akamshawishi kujiunga katika bendi yake ya Orchestra Safari Sound (OSS) ambayo ilikuwa ikiongozwa na Supreme  Ndala Kasheba aliyekuwa akipiga katika staili ya ‘Dukuduku’ nay eye Gurumo akaingia na staili ya ‘Ndekule’
Alijiunga na OSS akifuatana  na wanamuziki wawili toka  Mlimani Park akina Abel Bartazar na Kassim Rashid ‘Kizunga’ na kutoka na nyimbo za ‘Chatu mkali’ na ‘Bwana Kinyogoli’
Bendi ya OTTU ilikuwa bado inamuhitaji kurudi ndipo mwaka 1990 uongozi ulifanikiwa kumrudisha katika bendi hiyo ambayo tayari  ilikuwa ilikuwa  imebadili jina kuwa  JUWATA.
Enzi za ujana wake ‘Ubitozi’ wakati huo, Gurumo alipitia mambo mengi ya ujana yakiwemo ya  kuvuta sigara na  alikuwa mywaji wa pombe kupindukia ‘cha Pombe’  Tabia hiyo ilikifikia kukorofishana na mama yake mzazi aliyetishia hata kumutolea  ‘radhi’ kama angeendekeza ulevi.
Mkewe Pili naye alikwaruzana kila mara juu ya hiyo ya ulevi uliokithiri  na aliwahi kutishia kuomba talaka.
Hatimaye mwaka 1982, akaamua kumshinda ‘Shetani’ akaachana na ulevi kwa shinikizo la mama yake na mkewe.
Mzee huyu mwenye historia ndefu ya muziki na maisha yake kwa ujumla, amekuwa kiongozi katika bendi hiyo na anasema furaha aliyonayo ni kuona pale pamoja na umri wake kuwa mkubwa akiwa na msondo ngoma, amekwisha tunga  na kuimba nyimbo nyingi na kuzirekodi katika Studio zikiwemo za ‘Mama nipeleke kwa Baba’ Mwanangu acha Wizi, Wosi wa Baba na nyingine nyingi.
Muhidin Maalimu Gurumo amesema kwamba hana muda mrefu kabla ya kutangaza kustaafu fani ya muziki kutokana na hali yake ya kiafya halikadharika umri wake kumtupa mkono.
Anasema atakapostaafu atajikita katika kuwasaidia vijana ili atimize ndoto yake ya kujenga Chuo cha muziki katika shamba lake  lililopo Masaki wilayani Kisarawe, iwapo atapata wafadhili wa kumsapoti adhma yake.
Mzee huyo anasema mazoezi ni muhimu kwa kila binadamu. Yeye hulazimika kujikongoja kwenda kuimba katika bendi yake ya Msondo Ngoma. Wakati mwingine hulazimika huimba akiwa amekaa kwenye kiti. “Nja kali, nikienda huko pamoja na mazoezi ninayopata, pia huwa ninaambulia posho, inayoniwezesha kujikimu kimaisha” Mzee Gurumo  anasema kwa uwazi.
Gwiji huyu ametunga nyimbo zaidi ya 54 ambazo anasema zilizong’ara na kupendwa na watu japo yeye anasema kwamba hazina faida yeyote. Analalama  kwa kusema kuwa hapati hata senti tano toka katika nyimbo zake hizo. Hivyo anawaomba wadau na  wasamaria wema kumsaidia ili aweze kuzirekodi upya nyimbo hizo ili ziuzwe na yeye aweze kunufaika.
Kama walivyowahi kutamka wanamuziki wengine wa zamani, Mzee Gurumo naye amewasisitiza vijana wa muziki wa kizazi kipya kujifunza kutumia ala za muziki, ili kuweka kumbukumbu ya kazi zao kuwa endelevu kwa vizazi vijavyo.
Mzee Gurumo anamalizia kwa kusema anaomba serikali, mawaziri, wabunge na wadau  wote  wamuangalie kwa jicho la  huruma, kwa kumsaidia kufuatia  hali yake ya maradhi yanayomkabiri, na kwamba hana msaada mwingine, akisisitiza kuwa  wasisubiri hadi afe.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment

Wednesday, February 27, 2013

ALFA NA OMEGA YA MAQUIS

 BAADHI YA WANAMUZIKI WA MAQUIS DU ZAIRE TOKA KUSHOTO, SULEIMAN MBANA' 'COX', MBUA MAKONGA 'ADIOS', MUJOS WA BAYEKE, KAINGILILA MAUFFI, DEKULA KAHANGA, ISSA NUNDU MUKUMBULE LOLEMBO'PARASHI' NA MUKUNA ROY.
 NGUZA VICKING AKILIKUNG'UTA SOLO NA NYUMA YAKE NI MWIMBAJI ABOUBAKAR KASONGO MPINDA 'CLAYTON'
 ABOUBAKAR KASONGO MPINDA AKIIMBA NA NYUMA YAKE NI MPIGA GITA LA RHYTHM, MULENGA KALONJI 'VATA'
 KASONGO MPINDA 'CLAYTON' AKIWA NA MAPACHA KYANGA SONGA NA KASSALO KYANGA (KUSHOTO)
 WACARAZA MAGITA DEKULA KAHANGA 'VUMBI NA ILUNGA BANZA 'MCHAFU'(KUSHOTO) WAKIONESHA UMAHIRI WAO KWA KUCHARAZA 'MIPINI' SAKAFUNI.
 MBWEMBWE ZA MPIGA TUMBA SIDY MORRIS ' SUPER  KONGA' AKIPIGA TUMBA HIZO KWA KUTUMIA MIKONO NA MGUU
 MPULIZAJI WA TARUMBETA NKASHAMA KANKU KELLY AKIPULIZA KWA HISIA KALI.
WAIMBAJI WA MAQUIS DU ZAIRE KASONGO MPINDA 'CLAYTON NA MUTOMBO LUFUNGULA 'AUDAX'


March , 2013

MAQUIS du ZAIRE ni bendi ambayo ‘iliwatesa’ Watanzania kwa kuwaporomoshea burudani za  muziki wa dansi maridhawa katika kumbi mbalimbali hapa nchini.

Kwa wale waliokuwa vijana kati ya miaka ya 1970 na 1990, katu hawawezi kuisahau bendi hiyo ambayo iliingia hapa nchini kwa kishindo kikubwa ikitokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (Zaire) wakati huo.


Mwaka 1981, niliwahi kufanya mahojiano maalumu na mmoja wa viongozi wa bendi hiyo Chimbwiza Mbangu ‘Nguza Vicking’ ambaye alinipa wasifu wa bendi hiyo ya Maquis du Zaire.

Kwa kuwa wasifu huo uandikwa na kuchapishwa katika gazeti la serikali la Nchi Yetu la kila mwezi, ambalo lilikuwa likuzwa kwa senti 30, likitolewa na mwajiri wangu wakati huo, Idara ya habari (MAELEZO).

Hivyo basi  si vibaya nikirejea kuwapasha wale ambao hawafahamu na kwa waliosahau, nichukue muda wenu kwa kuwapa wasifu wa bendi hiyo tangia ilivyoanzishwa hadi kutoweka kwake  katika taswira ya muziki.

Historia ya bendi hiyo inaanzia mwaka 1960 kwa waliokuwa vijana wa wakati huo katika mji wa Kamina huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (Zaire), walioungana na kuunda bendi yao wakaiita Super Theo.

Bendi hiyo ilitoa burudani tosha kwa wapenzi wa muziki  wa Kamina  na vitongoji vinavyouzunguka mji huo, baadaye wakaibadilisha jina kuwa  Super Gabby.

Katika kile kilichoelezwa na uongozi wa Super Gabby kuwa ni kuleta mageuzi katika muziki, bendi hiyo mwaka 1972, ilibadili jina rasmi na kuwa Maquis du Zaire.

Maquis du Zaire iliingia hapa Tanzania mwaka huohuo wa 1972, kwa mwaliko wa mfanyabishara maarufu Mzee Batengas. Walianza kutumbuiza kwa mkataba katika ukumbi wa Mikumi Tours uliokuwa maeneo la Tazara  Buguruni, jijini Dar es Salaam.

Baada ya  kumaliza mkataba wao waliachana na Mzee Batengas,  wakaenda kupiga muziki katika Klabu ya Hunters kwa  kipindi kifupi. Kisha viongozi wa bendi hiyo wakafanya mazungumzo na mfanyabiashara Hugo Kisima aliyekuwa akimiliki wa  ukumbi wa Safari Resort  maeneo ya Kimara.

Mnamo mwaka 1977 Maquis du Zaire waliamua kuongeza nguvu kwa  kuimarisha kikosi chao. Hivyo uongozi huo ulimtuma Tchibangu Katayi ‘Mzee Paul’ kwenda Congo kutafuta wanamuziki wapya.

‘Mzee Paul’  alibahatika kuwachukuwa akina Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’, Kanku Kelly, Ilunga  Banza ‘Mchafu’, Mutombo Sozy na  mnenguaji Ngalula  Tshiandanda. Wakati huo walikuwa wakicheza katika mtindo wa ‘Chakula Kapombe’ ambao kwa watanzania ulikuwa mpya na ukapendwa mno na mashabiki.


Kufika kwa wanamuziki hao kulileta mabadiliko makubwa sana katika muziki husuani tungo nzuri za Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’ ambaye yaelezwa kuwa ndiye aliyeleta mapinduzi makubwa ya muziki hapa nchini Tanzania.

Maquis du Zaire wakaazisha mtindo mwingine wa ‘Kamanyola’, mtindo uliowapagaisha  wapenzi na wadau toka pembe zote za jiji la Dar es  Salaam. Mpulizaji wa Tarumbeta  Mwema Mudjanga ‘Mzee Chekecha’ alikuwa akiwahamasisha wapenzi wake akitoavibwagizo vya  “cheza Kamanyolaa.. ,cheza ukijidai’ cheza  Kamanyola bila jasho…”

Mwaka huo wa 1977 mwishoni  Maquis  walimaliza mkataba na wakaondoka kwa Hugo Kisima. Bahati nyingine ikawaangukia tena kwani  walisaini  mkataba mwingine na  Mzee Makao aliyekuwa akimiliki ukumbi wa Savannah,  maeneo ya Ubungo.

Wakiwa Savannah, walianzisha mitindo ya Sanifu na Ogelea piga mbizi baadaye ukumbi huo ukaitwa White House. Ikumbukwe kwamba  wakati huohuo Maquis pia ilikuwa ikipiga  kwenye ukumbi wa Mpakani, maeneo ya Mwenge. Ukumbi wa  Mpakani  baadaye ulibadilishwa jina kuwa   Silent Inn.  Kisha kuishia kuwa Kanisa.

Mwishoni mwaka 1978 waliamua kuimarisha tena kikosi chao kwa kuwaleta wanamuziki wengine wapya kutoka Congo ambao ni akina Kabeya Badu, Kalala Mbwebwe, Ngoyi Mubenga na  Khatibu Iteyi Iteyi.


Maquis du Zaire ilikuwa ikiongozwa na wanahisa akina Chinyama Chiyaza ‘Chichi’, Chibangu Katayi ‘Mzee Paul’, Chimbwiza Mbangu Nguza ‘Nguza Vicking’, Mutombo Lufungula ‘Audax’ na Mbuya Makonga ‘Adios’.

Chini  ya uongozi huo miaka ya 1980 mafanikio makubwa yalionekana. Mojawapo ni lile la kuanzisha Orchestra Maquis Company (OMACO). Kampuni hiyo ilikuwa ikimiliki shamba la matunda, wakilima kwa kutumia matreka yao maeneo ya Mbezi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam. Mazao yao walikuwa wakiyapeleka na kuuza katika Soko  Kuu la Kariakoo jijini Dar es Salaam.

OMACO pia  ilimiliki mradi mwingine wa viwanja  tisa na nyumba kadhaa maeneo ya Sinza na pia waliwahi kuingia mkataba wa kuitangaza kampuni ya magari makubwa ya SCANIA.

Vijana wa wakati huo watakumbuka jinsi ukumbi wa White House ulivyokuwa ukifurika watu kila siku za Jumamosi, kuwashuhudia vijana wa Maquis du Zaire waliokuwa watanashati na nidhamu ya hali ya juu wakiwa jukwaani wakifanya vitu vyao.

Enzi hizo ilikuwa ukiingia katika ukumbi huo wa White House, mbele yako macho lazima yakutane na mbao zilizo nakshiwa kwa maandishi ya majina ya wanamuziki wote na kukomelewa juu ya mwembe uliokuwa katikati ya ukumbi huo.

Maquis du Zaire ambayo ilikuwa ikipiga muziki mara moja kwa wiki, ilikuwa ikifika usiku wa manane, wanasisitisha muziki kwa muda  na kusikika kipaza sauti kikiuliza “Wapenzi mumekuja na miswakii?  Wapenzi walikuwa wakijibu “ndiyooooo…” Wanaelezwa dawa ya meno ipo hapo. Watu wengi hawakuwa na haja ya kuchukua teksi kurudi nyumbani kwani muziki wa Maquis du Zaire ulikuwa unarindima  hadi alfajiri, muda ambao mabasi ya UDA ya Ikarus yalikuwa yameanza kazi.


Bendi hiyo ikiwa hapa nchini ilikuwa ikipiga na kucheza katika  mitindo  mbalimbali kwa nyakati tofauti. Mitindo hiyo ilikuwa ya Chakula kapombe, Kamanyola, Bishe Bishe, Zembwela, Chekecha na Ogelea Piga mbizi.

Mwema Mudjanga ‘ Mzee Chekecha’ ndiye aliyekuwa akinogesha zaidi mitindo hiyo. Alikuwa kivutio kikubwa ukumbini licha ya kazi yake ya  kupuliza tarumbeta, aliweza kuwainua vitini wapenzi kwenda kucheza, akitumia  vibwagizo vya “Chekeee….  Chekechaaa”  “Tusangalaa”, “Aima imaa”,  ‘Bishe bishee”, “Saa… Sanifuu”,  “cheza Kamanyolaa”  “cheza kwa maringo”, “ Cheza  ukijidai” na mengine mengi.

Maquis du Zaire wakati huo  ilikuwa imesheheni wanamuziki zaidi ya 40 wenye vipaji vilivyopishana. Kwa idadi hiyo, laiti kama wangelikuwa na tamaa, wangeliweza kupiga muziki katika kumbi tatu tofauti kwa wakati mmoja.

Nina uhakika kwamba msomaji wangu unashauku ya  kujua au kukumbushwa kikosi kamili kilichokuwa kinatengeneza Maquis du Zaire wakati huo. Nikianza na safu ya waimbaji walikuwepo akina Mbuya Makonga ‘Adios’, Mutombo Lufungula ‘Audax’, Mukumbule Lolembo ‘Parashi’, Kabeya Badu, Kalala Mbwebwe, mapacha Kassalo Kyanga na  Kyanga Songa.
Wengine walikuwa  Kiniki Kieto, Abubakar Kasongo Mpinda ‘Clayton’, Mbombo wa Mbomboka, Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’, Tshimanga Kalala Assosa, Kabeya Badu, Masiya Radi ‘Dibakuba kuba’,  Issa Nundu na waimbaji wa kike  Tabia Mwanjelwa, Rahma Shaari na Anna Mwaole.

Wapiga gita  la solo alikuwepo  Chimbwiza Nguza Mbangu ‘Nguza Vicking’ ambaye kwa umahiri wake wa kulicharanza gita hilo, wapenzi walimpachika cheo cha juu kabisa jeshini cha   ‘Field Marshal’.
Wengine katika gitaa hilo  walikuwa akina Ilunga Lubaba, Dekula Kahanga ‘Vumbi’ na Mbwana Suleiman ‘Mbwana Cox’.

Gitaa la rhythm walikuwepo Mulenga Kalonji ‘Vata’, Omari Makuka na Steven Kaingilila Mauffi. Bila kuwashau akina Mbambu Kazadi, Mondo Mondonde na  Nawayi Kabwila.

Gitaa  zito la besi lilikuwa likiungurumishwa na Ilunga Banza ‘Banza Mchafu’ ambaye aliyejizolea umaarufu mkubwa kwa kulicharaza gita hilo  akiwa kajitwisha kwenye upara uliozungushiwa simbi kichwani kwake. Wengine walikuwa Ibrahimu na Mujos wa Bayeke.

Kama nilivyokujuza hapo awali kwamba bendi hiyo ilikuwa imejaza mseto wa vipaji mbalimbali. Kwa upande wa wapuliza Saxophone ‘mdomo ya bata’ walikuwepo akina Mafumu Bilali ‘Bombenga/‘Super Sax’,  Khatibu Iteyi Iteyi,  Alex Kanyimbo,  Akulyake Suleimani ‘King Mallu’, Roy Mukuna ‘Mukuna wa Mukuna’, Chibangu Katayi , Comson Mkomwa na  Majengo Selemani.

Wapuliza tarumbeta walikuwepo akina Mwema Mudjanga ‘Mzee Chekecha’ Nkashama Kanku Kelly,  Mioma wa Mwamba ‘Mzee Tito’, Kayembe Ndalabuu ‘Trumbloo’, Mpoyo Kalenga, Berry Kankonde,  Kaumba Kalemba,  Ngoi Mubenga, Ilunga Ngoi ‘Bizos’, Morgan Machege na Ngenda Kalonga.
Vijana hao kwa pamoja walikuwa wakitoa burudani maridadi  wakti mwingine walikuwa wakijitwisha tarumbeta zao vichwani wakilishambulia jukwaa, huku wakicheza kwa staili za aina yake ukumbini humo.

Madoido na mbwembwe hizo, ziliwavutia  wapenzi wengi na kupenda kuhamishia viti vyao wakisogea  sehemu iliyokuwa karibu, ili kushuhudia vijana hao wakifanya maajabu ya kuchezea vyombo hivyo.

Pamoja na uimbaji  Mbuya Makonga ‘Adios’  alikuwa mbonyezaji  wa kinada  huku Mutombo Sozzy  akizicharaza drums akisaidiana na  Matei Joseph.  Tumba zilikuwa zikigongwa na Siddy Morris ‘Super Konga’ na Pulukulu Wabandoki Motto.

Walikuwepo na wanenguaji  mahiri  ambao walikuwa wakitoa burudani za pekee akina ‘Washa Washa’, Dulla ‘Panga Panga’, Wandema Rashid, Anna Mganga, Kinacho, Mwajuma, Frida Shirima,  Zuwena na  Ngalula Tshiandanda, wakiongozwa na Nkulu Wabangoi.

Ikiwa White House bendi hiyo ilitoka na vibao vingi vikiwemo vya Double double, Clara, Kyembe, Maiga, Mpenzi Luta, Mwana yoka ya Babote, Ngalula, Nasononeka, Nimepigwa ngwala, Promotion, Ngalula, Karubandika na Noelle Bonane wimbo ambao ulikuwa ukipigwa mahsusi nyakati za Krimasi na mwaka mpya.

Zingine zilikuwa Dora mtoto wa Dodoma, Balimwacha, Malokelee, Promotion, Seya, Sophia, Sumu ya mapenzi, Sababu ya nini, Zowa, Uba, Safari ya Mbeya, Wakati nikiwa mdogo na nyingine nyingi zisizo idadi.
Kuna msemo usemao “Cha kuazima hakistiri maungo”  msemo huo uliisibu bendi ya  Maquis du Zaire baada ya kiungia katika maelewano ‘hafifu’ na mmili wa ukumbi  wa White House hadi kulazimika kuondoka wakiacha ukumbi huo ukibadilishwa kuwa gereji hadi leo.

Baadaye bendi hiyo ikabadilishwa jina na kuwa Maquis Original wakipiga muziki katika kumbi za Wapiwapi’s pale maduka mawili, Chang’ombe na CCM Kata ya 14 Temeke, kabla ya kuhamia ukumbi mpya kwa wakati huo wa Lang’ata pale  Kinondoni.

Maquis Original ilileta wanamuziki  wengine toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo muda mfupi kabla ya mpiga gitaa la solo, Dekula Kahanga ‘Vumbi’ kuondoka kwenda Stockholm nchini Sweden.

Wanamuziki hao walikuwa Kivugutu Motona Chatcho (Solo), na waimbaji Freditto Butamu na Luhembwe Mwahitwa ‘Bobo Sukari’.

Walitikisa ukumbi wa Lang’ata  kwa nyimbo zao kali za Mangolibo, Mayanga, Makumbele, zikisindikizwa na wimbo wa Ngalula ambapo wakati wa chorus katika wimbo huo, Tshimanga Assosa alikuwa akimpandisha mori mpiga gita la solo Dekula Kahanga ‘Vumbi’ akimwita “vumbiii… Vimbiiii… Vumbiii…” Nyimbo za Maquis Original zilikuwa  zikipigwa na kutamba kwa staili za ‘Washawasha’ na ‘Sendema’.

Maquis Original ikiwa Lang’ata, kuna shabiki mmoja aliyejulikana kwa jina la ‘Magoma moto’  ambaye  alikuwa kivutio kikubwa kwa wapenzi wa Maquis. Alikuwa akiachwa uwanja akionehsa uhodari wake wa kucheza mtindo wa  ‘Sendema’  huku akiwa kajitwisha chupa yenye Bia juu ya kichwa chake.

Ni miaka takriban 23 toka  jina la Maquis litoweke masikioni mwa wadau na wapenzi wa muziki wa dansi baada ya kusambaratika katika  miaka ya 1990, ikiwaachia simanzi na majonzi wapenzi wake yasiyokwisha hadi leo.
Lakini Tshimanaga Kalala Assosa ‘mtoto mzuri’ baadaye alitumia weledi wake katika muziki kwa kuienzi  jina la Maquis kwa kuanzaisha bendi ya ‘Bana Maquis’  ambayo hupiga na kukumbushia nyimbo zilizopigwa na Maquis  du Zaire na Maquis Original.

Ikumbukwe kwamba idadi kubwa miongoni mwa wanamuziki wanaotajwa humu, wameshatangulia mbele za haki.

Wengine ni wale wanaumwa maradhi mbalimbali akina Aboubakar Kasongo Mpinda ‘Clayton’, Mbombo wa Mboka na Mutombo Lufungula ‘Audax’

 Mungu aziweke roho zao pahala pema peponi waliotangulia mbele za haki na awape tahfifu wanaoumwa, Amen.